Saturday, June 2, 2012

Mtambue Mwinjilisti wa Kimataifa, JOHANNES AMRITZER na Mkutano Mkubwa wa Sherehe za Ishara Na Miujiza

Mchungaji na Mwinjilisti wa kimataifa, Johannes Klaus Amritzer ni mme wa mke mmoja aitwaye Maria na wana watoto wawili, Alicia na Adam.

Alizaliwa Australia akahamia Sweden akiwa na umri wa miaka 4. Ametembea sana katika Dunia hii kiasi kwamba inakadiriwa kuwa huwa yuko katika safari za kiutumishi siku 250 kati ya siku 365 za mwaka. Kama hiyo haitoshi, amewahi kuwa na anuani 22 tofauti kwa sababu ya kutembea maeneno mengi humu Duniani akimtumikia Mungu. Toka Mei 2009 anaishi Tullinge, Kusini mwa mji mkuu wa Sweden, uitwao Stockholm.

Ni Mwinjilisti wa sherehe/ mikutano , mwanzilishi wa SOS MISSION INTERNATIONAL, mpanda makanisa, Mchungaji Kiongozi kanisa la SOS INTERNATIONAL la Stockholm, Sweden. Pia ni mwalimu katika chuo cha Biblia cha huduma yake ya SOS MISSION INTERNATIONAL, Mwenyekiti wa uongozi wa mtandao wa utume wa Kikristo wa nchi za Scandinavia, mwandishi wa vitabu kadhaa na majarida na mnenaji anayependwa wa makongamano huko Ulaya, USA, Afrika na Asia.


Johannes and Maria Amritzer

Johannes na Maria Amritzer wameanzisha huduma hii mwaka 1996. Mpaka sasa ina watendaji 150 kote Duniani. Maono, maombi na shauku ya kuona mpenyo unatokea bado ni uleule lakini kila kitu kinaendelea kukua.
Makanisa 340 yamekwisha pandwa ikiwa ni matokeo ya Mikutano ya Sherehe 50. Makumi elfu ya watu wamempokea Yesu, kubatizwa katika Roho Mtakatifu na Maji. Yesu alifanya miujiza mingi ya ajabu, vipofu wanaona, viziwi wanasikia na viwete kutembea, kukimbia na kuruka.

Ofisi za huduma hii ziko Norway, Australia na Sweden na wanaendesha shule za mafunzo ya kimishionari Stockholm Sweden, Pittsburgh USA, Harar Ethiopia, Velingrad Bulgaria na Khon Kaen Thailand.

Neno la Johannes na Maria Amritzer, Raisi na mwanzilishi wa SOS MISSION INTERNATIONAL:

Pamoja na makanisa ya mahali pamoja katika pande zote za Ulimwengu huu, tunahubiri habari njema za Yesu Kristo kwa watu wasiofikiwa kupitia kampeni na sherehe za ishara na miujiza. Tunakuwa na semina za wachungaji ili kutengeneza watendaji wa kutosha katika maeneo hayo kuhakikisha ufuatiliaji na upandaji makanisa unaendelea kufanyika katika maeneo yote yasiyofikiwa ya Ulimwengu huu.

Kwa lengo mahususis la kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu, tunasamabaza Biblia na vitabu au machapisho ya Kikristo katika lugha za maeneo husika. SOS MISSION INTERNATIONAL ina msingi wake katika mtandao wa makanisa ya Sweden na USA na tunashirikiana na kila mtu aliye katika Movement ya kipentekoste ya kimataifa na familia ya kikarisimatiki pasipo kujali dhehebu.

HATA HIVYO BADO HUDUMA INAENDELEA KUKUA.

Mkutano wa Sherehe za Ishara na Miujiza

Mkutano utafanyika katika Viwanja vya Jangwani, kuanzia Jumatano tarehe 13 mpaka Jumapili tarehe 17 Juni 2012. Muda ni kuanzia saa 9:00 alasiri mpaka saa 12:30 jioni. Watu zaidi ya 50,000 wanatazamiwa kuhudhuria ukiwemo wewe. Kama imewahi tokea basi ni mara chache.

Watu wengi watampokea Yesu na kufunguliwa toka katika vifungo vya shetani. Usiache kufika huku ukijua unamhitaji Bwana Yesu ili akutoe wewe au nduguyo katika dhiki hiyo.

Waimbaji katika mkutano; Bendi ya huduma ya SOS MISSION itahudunu. Pia wenyeji kama Kinondoni Revival Choir, Temeke Revival Choir, The Reapers, Dar-Es-Salaam Gospel Choir, Upendo Nkone, Christina Shusho, Bon Mwaitege n.k. watakuwa wakimwimbia Mungu.


Bendi ya huduma ya SOS.







Kongamano la wachungaji la mpenyo wa kitume

Wachungaji na watumishi wengine wa Mungu watakuwa na kongamano pale City Christian Centre, Upanga kuanzia tarehe 13 – 15 Juni 2012. Wachungaji 1500 toka kote Tanzania wamepewa ufadhili na wengine wote watajigharimia kila kitu.

Wachungaji wanaendelea kujiandikisha na mpaka sasa idadi ni takribani 1500 tayari wamejiandikisha kuhudhuria kongamano la mpenyo wa kitume. Mchungaji yeyote ambaye bado, apige simu haraka sana ili kuona uwezekano wa kumsaidia kupata ufadhili huo kama nafasi zitakuwa hazijaisha.

Wageni kutoka Nje; Marekani, Sweden,Norway n.k.

Wakati wachungaji wakiwa kwenye kongamano asubuhi kuanzia saa 3 mpaka 7, kuna makundi 5 yatakuwa yakizunguka mitaani kuhubiri Injili katika vituo mbalimbali kama Mwenge, Karume, Mwembe yanga, Kariakoo, Ubungo, karibu vituo vyote vya daladala vya Morogoro road (Ubungo mpaka Jangwani ), katika shule, hospitali, magereza pia.

Wanakuja watu 190. 100 wanatoka kanisa linalochungwa na Mchungaji na mwinjilisti wa Kimataifa, Johannes Amritzer na wengine 90 wanatoka Marekani, Norway n.k. Ungana na jopo hili kuifikisha injili katika mitaa mbalimbali ya jiji hili la Dar-Es-Salaam linalomuhitaji Mungu sana.

Uhitaji wa watu wanaojitolea

Kuna uhitaji wa wahudumu, watafsiri, walinzi, washauri, wajenzi, waombaji n.k. Kama umeokoka na unamwamini Yesu una kazi ya kufanya ili wengine wamrudie Kristo. Tupigie simu ili uingie katika kundi la watumishi wengine wa Mungu wanaojitoa kuhakikisha kuwa kazi hii inafanikiwa.

IBILISI CHA MOTO AMEKIPATA, TUTAENDELEA KUKUJUZA KINACHOJIRI, USIENDE MBALI.

Cell: +255 714 50 36 38 / +255 762 441 719
Facebook page: Mkutano Mkubwa Wa Sherehe Za Ishara Na Miujiza 
Twitter:https://twitter.com/ISHARAMIUJIZA 

Tuesday, May 29, 2012

Mkutano Mkubwa sana wa Sherehe za Ishara na Miujiza; Dar-es-salaam.



Mkutano mkubwa sana kuwahi kufanyika jijini Dar-es-salaam hatimaye bado siku 14 yaani majuma mawili tushuhudie roho za watu wengi sana zikirejea tena kwa muumba wa vyote.

Kamati za maandalizi zinafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa kinachobaki iwe ni Bwana mwenyewe kuyagusa maisha ya watu; wakiokoka na wengi kufunguliwa toka katika vifungo vya yule mwovu Ibilisi.

Pitia  http://www.missionsos.org/en johannes_amritzer/ kuelewa ni nani huyo, Johannes Amritzer ambaye Bwana amekuwa akimtumia kwa injili ya mikutano mikubwa sana hapa duniani.